Kufuatia
 maagizo ya Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
 wa Tanzania aliyoyatoa hivi karibuni ya kusitisha safari za nje kwa 
Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na 
Ushirikiano wa Kimataifa imeanza kutekeleza maagizo hayo kwa kutoa 
maelekezo mahsusi kwa Balozi zake nje.
Wizara
 imezielekeza Balozi zote zilizopo maeneo mbalimbali duniani kujipanga 
ili kushiriki kikamilifu katika kuiwakilisha Serikali kwenye mikutano 
yote ya kimataifa na kikanda inayofanyika katika maeneo yao ya 
uwakilishi. Tanzania inazo Balozi 35; Balozi Ndogo tatu; Vituo viwili 
vya Biashara; na Konseli za Heshima 17 katika nchi mbalimbali. Hizi zote
 zitahusika katika kuendeleza utekelezaji wa Diplomasia yetu ya Uchumi 
na uwakilishi wa maslahi ya nchi yetu.
Aidha,
 hadi sasa Mikutano ambayo tayari imefanyika na Balozi zetu kuwakilisha 
ni pamoja na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) 
unaoendelea nchini Malta na Mkutano wa Mawaziri wanaoshughulikia masuala
 ya Habari wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) 
unaofanyika nchini Lesotho.
Aidha,
 Wizara inatoa wito kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kuwasilisha
 mapema taarifa za mikutano inayohusu sekta zao ili kutoa fursa kwa 
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuzifanyia kazi kwa 
wakati ili kuhakikisha ushiriki wa Tanzania unakuwa wenye tija kwa 
taifa.
Wizara
 ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaungana na wadau wengine 
kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa hatua anazozichukua za kuleta ufanisi 
mkubwa wa kazi na kubana matumizi ili kuiwezesha Serikali kuwahudumia 
wananchi kikamilifu.
Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
27 Novemba, 2015
 
 
 
 
 
 

 
 
0 comments:
Post a Comment