Meneja Mradi
TANESCO Mhandisi Simon Jalima (wa pili kushoto) akimwonyesha Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi
Kalemani (wa pili kulia) moja ya mtambo unaopokea gesi kutoka mtwara na
kuisambaza mpaka kituo cha Ubungo alipofanya ziara ya kuona maendeleo ya mradi
huo leo katika eneo la mradi Kinyerezi jijini Dar es Salaam, wa kwanza kulia ni
Naibu Mkurugenzi Mtendaji Tanesco Bw. Decklan Mhaiki.
Meneja Mradi
TANESCO Mhandisi Simon Jalima (wa pili kushoto) akimtembeza Naibu Waziri Wizara
ya Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani (wa pili kulia) kumwonyesha mitambo
mbalimbali ya uzalishaji wa umeme uliyopo katika kituo hicho cha Kinyerezi I, jijini
Dar es Salaam.
Mmoja wa wataalamu wa kuendesha mitambo inayosambaza nishati ya umeme uliyozalishwa kwa kutumia gesi (Shift Supervisor) Bw. Mohamed Lanzi akimwonyesha Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani (wa kwanza kulia) mtambo wa usambazaji wa umeme wa Morogoro unaotokea Kinyerezi I namna wanavyouendesha.
Meneja
Mradi wa Kinyerezi Extension kutoka
Kampuni ya Sumitomo Japan Bw. Shoji Watanabe akimweleza Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi
Kalemani ni kwa muda gani mradi huo utakamilika mara baada ya kupewa mkataba wa
kuanza kazi hiyo, leo Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri
Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani (wa kwanza kulia) akitoa
maagizo kwa Meneja Mradi wa Kinyerezi
Extension kutoka Kampuni ya Sumitomo Japan Bw. Shoji Watanabe (wa kwanza
kushoto) alipokuwa akigua eneo la mradi huo leo Kinyerezi jijini Dar es Salaam,
(wa pili kulia) ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Tanesco Bw. Decklan Mhaiki.
Na Anitha Jonas –MAELEZO
Tarehe 14/12/2015
Dar es Salaam.
Wizara ya Nishati na Madini
imewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha
uzalishaji wa umeme katika Mradi wa Kinyerezi I na Kinyerezi II unakamilika
ifikapo mwezi Februari 2016 na kuanza
kufanya uzalishaji ilikuongeza kiasi cha nishati ya umeme kufikia zaidi ya Megawati 100.
Agizo hilo lilitolewa leo na
Naibu Waziri, Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani alipofanya ziara
yake katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya Gesi cha Kinyerezi
jijini Dar es Salaam,hii ni baada ya kuelezwa kuwa kituo hicho kwa sasa
kinazalisha 70 Megawati za umeme ambaohautoshelezi kwa matumizi ya watanzania.
“Watanzania wamechoshwa na mgao
wa umeme na wanaimani kubwa na uzalishaji wa kituo hiki cha kuzalisha umeme kwa
kutumia gesi hivyo wanatarajia umeme wa uhakika katika kufanya shughuli
mbalimbali za uzalishaji na kujipatia kipato”,alisema Dkt.Kalemani.
Hata hivyo Dkt. Kalemani aliwapongeza
watendaji wa TANESCO na wakandarasi wanaosimamia uendeshaji wa mitambo hiyo ya
uzalishaji huku akiwasihii waongeze jitihada za dhati kwani watanzania bado
hawaridhishwi na kiasi cha umeme kinachozalishwa kwa sasa.
Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini Mhandisi Omari Chambo alisema kuna mradi mpya uitwao
Kinyerezi Extension unakaribia kuanzishwa hivi karibuni ambao utazalisha Megawati
345 za umeme na kupitia mradi huu uzalishaji wa umeme utaongezeka kwa kiasi
kubwa.
“Tutajitahidi kwa sasa umeme
usikatike mara kwa mara na jitihada za kusafisha mitambo miwili ya phase I na
Phase II inafanyika na itakapokamilika tunatarajia kuzalisha zaidi ya Megawati
140 za umeme na usafishaji wake unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi
Desemba mwaka huu”,alisema Mhandisi Chambo.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji
TANESCO Bw.Decklan Mhaiki alisema mradi wa Kinyerezi Extension ambao utagharimu jumla ya kiasi cha Dola Milioni 340 unatarajia
kuanza hivi karibuni mara baada ya kukamilika kwa Mkataba na malipo ya 15% kwa
mkandarasi.
Pamoja na hayo wizara ya Nishati
na Madini imetoa angalizo kwa watendaji wote wanaozalisha umeme kwa kutumia
maji walinde vyanzo vya maji na kuacha kutumia maji hayo kwa matumizi mengine
kama ya kilimo.
Uzalishaji wa umeme kwa kutumia
Nishati ya Gesi utasaidia kupunguza gharama za watumiaji wa umeme pamoja na
kushusha gharama za uzalishaji.