ENEO LA LEBANON KATIKA SOKO LA KIMATAIFA LA SAMAKI LA FERI JIJINI DAR NI HATARI KWA UCHUMI.
Friday, November 06, 2015
                                      Maoni: 
                                      0
Na Dotto Mwaibale
ENEO
 la Lebanon katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri ambalo lipo 
jirani na Ikulu jijini Dar es Salaam limedaiwa kuwa ni hatari kwa 
wafanyabiashara wa soko hilo na kuwa linadhohofisha uchumi kutokana na 
kukithiri kwa watu wasio rasmi.
Hayo
 yamebainishwa na Mwezeshaji wa Sheria wa soko hilo, Asha Malenda wakati
 akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi 
wanaotembelea masoko mbalimbali ya Manispaa ya Ilala kuona jinsi gani 
vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia umepungua katika soko hilo baada ya 
Shirika la Equality for Growth (EfG) kutoa mafunzo ya kupinga ukatili 
katika masoko hayo.
"Tunachangamoto
 kubwa sana katika soko letu la Feri tunayoipata kutoka eneo la Lebanon 
lenye mwingiliano wa watu wasio rasmi kutoka nje ya soko ambao ni kama 
wamejianzishia soko lao na wamekuwa na maamuzi yao lakini viongozi wa 
soko la Feri wanashindwa kuwachukulia hatua hali ambayo inatudhalilisha 
sisi wafanyabiashara hasa mama lishe na kuharibu uchumi wa soko letu" 
alisema Malenda.
Alisema
 wengi wa watu waliopo katika eneo hilo lisilo rasmi wamekuwa wakifanya 
biashara kiholela huku wakipika vyakula katika maeneo yanayoweza 
kuhatarisha afya ya mlaji wakati katika soko hilo kuna eneo maalumu la 
mama lishe na wengi wa watu hao wakienda kula eneo hilo rasmi wamekuwa 
hawalipi fedha na wakibanwa kulipa wanadiliki kutoa visu na silaha za 
jadi kuwatishia wanaodai.
"Eneo
 hilo la Lebanon ni hatari na kinachoshangaza linatizamana na Ikulu 
lakini hakuna hatua yoyote ya makusudi inayochukuliwa na viongozi wetu 
na linapopelekwa kwa viongozi wa kisiasa wanadai waachwe kwani ndio 
wapiga kura wao" alisema Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Bakari 
Said.
Said
 alisema katika soko hilo kuna changoto nyingi za udhalilishaji wanawake
 kwa kushikwa katika maungo yao lakini kupitia EfG wamejitahidi 
kupunguza changamoto hizo kwani wasaidizi wa sheria waliopatiwa mafunzo 
na shirika hilo wanajitahidi kuupenyeza ujuzi waliopata kuifikishia 
jamii ambayo imeanza kuelewa kuhusu vitendo hivyo.
Aliongeza
 kuwa uvaaji wa nguo za kubana na kuacha vifua wazi kwa upande wa 
wanawake pia ulikuwa ukichochea kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji 
uliokuwa ukifanywa na vijana wasio rasmi katika eneo hilo la Feri ambao 
hawana makazi na maisha yao yapo Feri lakini baada ya kufikiwa na 
mafunzo ya EfG hali hiyo imepungua kwa asilimia 80.
Mwezeshaji
 Fatuma Saijali alisema changamoto kubwa iliyopo hivi sasa katika soko 
hilo ni kuzuiliwa kupika chakula katika eneo hilo la Feri lakini wakati 
huo huo kuna kundi la wanawake wamekuwa wakiingiza chakula kutoka 
majumbano kwao na kukiuza hivyo kuharibu soko lao la chakula.
Mwenyekiti
 wa Kamati ya Soko hilo, Ali Kibwana alisema mafunzo waliyopata kupitia 
EfG yamesaidia sana kupunguza vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika
 soko hilo na kila mtu anayebainika kujihusisha na vitendo hivyo amekuwa
 akiitwa na kukanywa na kama akiendelea kuwa mkaidi anachukuliwa hatua 
nyingine kwa kufuata kanuni na sheria.
Kamanda
 wa Ulinzi na Mazingira wa Soko hilo, Nurdin Hassan amesema hali katika 
soko hilo ni nzuri kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na EfG ya kufanya 
semina na matamasha ya uhamasishaji hivyo kuifanyajamii kuelewa kuhusu 
vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Ofisa
 Ufuatiliaji na Tathmini wa EfG, Shaban Rulimbiye alisema Shirika hilo 
linaendesha mradi wa miaka mitatu wa Mpe Riziki si Matusi wenye lengo la
 kutoa elimu ya kupinga ukatili wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na 
udhalilishaji na nia zaidi mradi huo ni kuusambaza hadi katika maeneo 
mengine ya nchi.
 
 
 
 
 
 
 
 
0 comments:
Post a Comment