India
imeipatia Tanzania dola za Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya
maendeleo ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina nchi hizi mbili
Hayo
yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika dhifa ya
kitaifa aliyomwandalia mgeni wake, Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra
Modi.
“Tunaishukuru India ambayo imeonyesha utayari wa
kushirikiana nasi kiuchumi katika kilimo, TEHAMA, maji, Elimu, Afya na Ulinzi,”
amesema Rais Magufuli.Rais Magufuli pia amesema ushirikiano wetu na India
utatoa fursa kwa Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda kwani
katika ziara hii Waziri Mkuu ameambatana na wafanyabiashara takriban 50 ambao
wanaangalia fursa za kibiashara hapa nchini.
“India ni mdau wetu mkubwa wa kibiashara na uhusiano huu umekuwa ukikua kwani mauzo ya bidhaa
za Tanzania nchini India yameongezaka toka thamani ya dola za kimarekani milioni 187 mwaka 2005 hadi
dola bilioni 1.29 mwaka 2015,”alisema Rais Magufuli.Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa India itatoa fedha
kwa nchi ya Tanzania kwa ajili ya kilimo cha Dengu ambayo ni fursa ya ajira kwa
watanzania na kuinua kipato cha wananchi.
Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa kwake na miradi
ya India ikiwemo mradi unaojulikana kama Making
India, mradi ambao unatumia malighafi zinazopatikana nchini na kutumia
nguvu kazi ya nchini ambao utapunguza tatizo
la ajira katika Taifa la Tanzania.
Amebainisha kuwa India iko tayari kushirikiana na
Tanzania kwenye miradi ya gesi ikizingatiwa kuwa aina mbali mbali za gesi
zinazidi kugunduliwa hapa nchini. Katika suala la gesi India iko tayari kutoa utaalamu
na wataalamu kwa ajili miradi ya gesi.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa India , Mhe. Narendra
Modi ameishukuru Tanzania kwa ukarimu alioupata hapa nchini na akaahidi
kuendeleza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.Amesema India italeta watu wake, utaalaamu na
teknolojia yake kwa Tanzania, jambo ambalo litaongeza ushirikiano wa kiuchuni
kati India na Tanzania.
Waziri Mkuu huyo amemaliza ziara yake ya kiserikali ya siku mbili nchini na kuondoka kuendelea na
ziara katika nchi nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki.