Kama Bado Hujajiunga Nami, Unaweza Kujiunga Kwa Kubonyeza Like Hapa Chini Nikutumie Habari Moja Kwa Moja 
Wagombea wa CCM na Chadema wanaendelea kuchuana vikali kwenye mbio za 
urais baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza matokeo ya 
majimbo 113.
Hadi jana jioni kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na NEC, mgombea wa 
CCM, Dk John Magufuli alikuwa anaongoza kwenye majimbo mengi akifuatiwa 
na Edward Lowassa anayegombea kwa tiketi ya Chadema, akiungwa mkono na 
vyama vingine vitatu vya NLD, CUF na NCCR-Mageuzi.
Kwa mujibu wa matokeo hayo ya NEC, Dk Magufuli alikuwa amekusanya zaidi 
ya kura 2.4 milioni sawa na asilimia 57 katika majimbo hayo, wakati 
Lowassa, aliyehamia Chadema mwezi Julai, amepata kura zaidi ya 1.7 
milionisawa na asilimia 41.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, ni NEC pekee inayoruhusiwa kutangaza matokeo ya urais.
Mgombea pekee mwanamke kwenye uchaguzi huo kati ya makada nane kutoka 
vyama tofauti, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, anafuatia nyuma ya 
wagombea hao wawili, akiwa amepata zaidi ya kura27,000 ambazo ni sawa na
 asilimia 0.64.
Mgombea urais wa ADC, Chifu Lutasola Yemba anamfuatia kwa kuwa na 
asilimia 0.52 ya kura zote, chini yake akiwapo Hashim Rungwe wa Chaumma 
ambaye amekusanya asilimia 0.38 ya kura zote.
Janken Kasambala, anayegombea urais kwa tiketi ya NRA, amekusanya 
asilimia 0.09 ya kura zote, Macmillan Lyimbo, aliyesimamishwa na TLP 
(asilimia 0.07) na Fahmy Dovutwa wa UPDP (asilimia 0.07).
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, ambaye awali aliwahi kusema 
watatangaza mshindi ndani ya saa 72 baada ya kumalizika upigaji kura, 
jana aliwaomba wasimamizi wa uchaguzi kuongeza kasi ya kuwatumia matokeo
 ili wayatangaze.
Hata hivyo, vyama vinavyounda Ukawa jana vilitoa tamko la pamoja vikidai
 kuwa uchelewashwaji wa matokeo unatokana na uchakachuaji unaofanywa na 
kikundi cha chama tawala.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari jana
 kuwa kura zote zinazokusanywa kutoka majimboni, hupitia hoteli moja Dar
 es Salaam ambako kuna kikundi hicho na vijana ambao wanachakachua 
matokeo kabla ya kuyatuma NEC.
Lakini Jaji Lubuva amekuwa akijitetea kuwa NEC inatangaza matokeo kadri 
inavyoyapokea na hawana njama zozote dhidi ya chama chochote cha siasa.
Kwa upande wa matokeo ya ubunge, CCM ilikuwa imeshinda katika majimbo 
135, Chadema majimbo 34, CUF majimbo 22, NCCR-Mageuzi jimbo moja na ACT-
 Wazalendo jimbo moja kati ya 264.
 
 
 
 
 
 


 
 
0 comments:
Post a Comment