Mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza.
NA MWANDISHI WETU
MSHAMBULIAJI wa Simba, Hamis Kiiza, anatarajiwa kukabidhiwa zawadi
 yake ya Sh milioni 1/-ya Mchezaji Bora wa Mwezi na wadhamini wakuu wa 
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, kampuni ya mawasiliano ya Vodacom 
Tanzania, baada ya kuibuka kidedea Septemba.
Kiiza 
alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Septemba baada ya kufanya vema katika
 mwezi wa kwanza wa ligi hiyo, akiisaidia timu yake ya Simba kushinda 
mechi tatu mfululizo, huku Mganda huyo akifunga mabao matano, ikiwamo 
‘hat-trick’ katika pambano dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa,
 Dar es Salaam.
Kwa 
mujibu wa Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, Kiiza 
atakabidhiwa kitita chake hicho na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, 
Ian Ferrao, wakati wa mchezo wa Simba dhidi ya Majimaji Oktoba 31, mwaka
 huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Alisema
 kuwa kampuni yao itaendelea kutoa zawadi kwa wachezaji wanaofanya 
vizuri kila mwezi, ikiwa ni sehemu ya mikakati na mchango wao katika 
kuinua kiwango cha michezo, hususan soka nchini na kubadilisha maisha ya
 wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu.
“Katika
 kuendeleza mikakati yetu ya kuinua soka hapa nchini pamoja na kuboresha
 maisha kwa wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, 
Vodacom Tanzania, itamjaza kiasi cha Sh milioni moja mshambuliaji wa 
Simba, Hamis Kiiza kutokana na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa ligi 
hiyo kwa Septemba msimu huu,” alisema Nkurlu.
Juu ya
 tuzo hiyo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, 
ameishukuru na kuipongeza Vodacom Tanzania ubunifu huo wa kuwazawadia 
wachezaji wanaofanya vizuri kwani kitendo hicho huchangia kuendeleza 
vipaji na kuwahamasisha wachezaji kufanya vizuri zaidi na kuzisaidia 
timu zao.
“TFF 
tunaamini zawadi kama hizi zinazotolewa kwa Mchezaji Bora wa Mwezi, 
zinaweza kuwa chachu kwa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu kujituma zaidi 
kwa faida yao, klabu zao na soka la Tanzania kwa ujumla,” alisema.
 
 
 
 
 
 


 
 
0 comments:
Post a Comment