Pages

Ads 468x60px

Sunday, November 8, 2015

ENEO LA LEBANON KATIKA SOKO LA KIMATAIFA LA SAMAKI LA FERI JIJINI DAR NI HATARI KWA UCHUMI.


Mwenyekiti wa Kamati ya Soko la Samaki la Kimataifa la Feri, Ali Kibwana, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi wanaotembelea masoko mbalimbali ya Manispaa ya Ilala kuona jinsi gani vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia umepungua katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG) kutoa mafunzo ya kupinga ukatili katika masoko hayo. Kushoto ni Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Bakari Said.
Mwonekano wa sehemu ya soko la Samaki la Feri.

Na Dotto Mwaibale
ENEO la Lebanon katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri ambalo lipo jirani na Ikulu jijini Dar es Salaam limedaiwa kuwa ni hatari kwa wafanyabiashara wa soko hilo na kuwa linadhohofisha uchumi kutokana na kukithiri kwa watu wasio rasmi.

Hayo yamebainishwa na Mwezeshaji wa Sheria wa soko hilo, Asha Malenda wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi wanaotembelea masoko mbalimbali ya Manispaa ya Ilala kuona jinsi gani vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia umepungua katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG) kutoa mafunzo ya kupinga ukatili katika masoko hayo.

"Tunachangamoto kubwa sana katika soko letu la Feri tunayoipata kutoka eneo la Lebanon lenye mwingiliano wa watu wasio rasmi kutoka nje ya soko ambao ni kama wamejianzishia soko lao na wamekuwa na maamuzi yao lakini viongozi wa soko la Feri wanashindwa kuwachukulia hatua hali ambayo inatudhalilisha sisi wafanyabiashara hasa mama lishe na kuharibu uchumi wa soko letu" alisema Malenda.

Alisema wengi wa watu waliopo katika eneo hilo lisilo rasmi wamekuwa wakifanya biashara kiholela huku wakipika vyakula katika maeneo yanayoweza kuhatarisha afya ya mlaji wakati katika soko hilo kuna eneo maalumu la mama lishe na wengi wa watu hao wakienda kula eneo hilo rasmi wamekuwa hawalipi fedha na wakibanwa kulipa wanadiliki kutoa visu na silaha za jadi kuwatishia wanaodai.

"Eneo hilo la Lebanon ni hatari na kinachoshangaza linatizamana na Ikulu lakini hakuna hatua yoyote ya makusudi inayochukuliwa na viongozi wetu na linapopelekwa kwa viongozi wa kisiasa wanadai waachwe kwani ndio wapiga kura wao" alisema Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Bakari Said.

Said alisema katika soko hilo kuna changoto nyingi za udhalilishaji wanawake kwa kushikwa katika maungo yao lakini kupitia EfG wamejitahidi kupunguza changamoto hizo kwani wasaidizi wa sheria waliopatiwa mafunzo na shirika hilo wanajitahidi kuupenyeza ujuzi waliopata kuifikishia jamii ambayo imeanza kuelewa kuhusu vitendo hivyo.

Aliongeza kuwa uvaaji wa nguo za kubana na kuacha vifua wazi kwa upande wa wanawake pia ulikuwa ukichochea kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji uliokuwa ukifanywa na vijana wasio rasmi katika eneo hilo la Feri ambao hawana makazi na maisha yao yapo Feri lakini baada ya kufikiwa na mafunzo ya EfG hali hiyo imepungua kwa asilimia 80.

0 comments:

Post a Comment

 
Blogger Templates