Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo
asubuhi katika Ikulu ya Dar es Salaam amefanya kikao na Makatibu
wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu na
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutoa uelekeo wa
Serikali anayoitaka mara baada ya kuapishwa.
“Nataka Serikali iendelee kwa nguvu zote na katika kutekeleza dhana
ya ‘HAPA KAZI TU’ na viongozi kuzingatia na kukumbuka ahadi nilizotoa
ili zianze kuonekana na kufanyiwa kazi mara moja” Rais Magufuli amesema.
Katika Kikao chake, Rais ametoa mwongozo na kusisitizia kuwa ni
lazima kila mtendaji Serikalini kuuzingatia, kufuata sheria na taratibu
ili taifa lisonge mbele kwa ufanisi zaidi. Katika kikao hicho Rais
ameelekeza mambo kadhaa ambayo watendaji hao wanapaswa kuyasimamia,
kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili atakapo teua Baraza lake la
Mawaziri mambo hayo yawe tayari ili Mawaziri watakaoteuliwa waweze
kuyasimamia bila kukosa.
Mambo hayo muhimu ni kama ifuatavyo:
Kuanzia
mwezi Januari mwaka 2016, wanafunzi wote wanaoanza shule watasoma bure
bila kulipa ada, Katika jambo hili, Rais amewataka watendaji kuanza
kuliwekea mikakati tayari kwa utekelezaji Suala la mikopo ya wanafunzi
nalo lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji
mzuri zaidi Amefuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo
atakapolitolea suala hilo maamuzi mengine na kueleza kuwa shughuli zote
zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa
Tanzania wanaowakilisha nchi huko nje.
Pengine patokee jambo la dharura sana na hata hilo lazima kibali kitolewe na Rais au Katibu Mkuu Kiongozi. Badala yake Rais amewataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi wa Tanzania.
Katika Kikao hicho, Rais amemtaka Kamishna wa TRA, Ndugu Rished Bade
kusimamia kwa makini zoezi la ukusanyaji wa mapato nchini na
kuhakikisha kero ndogo ndogo kwa wananchi lianze kutekelezwa kama alivyo
ahidi kwa kufanyiwa kazi mapema zaidi.
Rais ameitaka TRA kukusanya mapato hayo kutoka kwa wafanya biashara
wakubwa zaidi na wale wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi
yoyote hapa Tanzania na kusisitiza kuwa katika Serikali hii wa kutoa
maamuzi vinginevyo zaidi ya haya ni yeye Rais ama Makamu wake.
Rais Magufuli pia ameagiza usimamizi katika suala la manunuzi ambalo
limekuwa likitumika vibaya na kuwa mwanya wa kuibia Serikali kwa watu
kuongeza bei ya vitu hata kama ni vya bei ndogo kabisa katika jamii.
“Ikitokea suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu,
watendaji watawajibishwa mara moja”. Rais amesema, na kuwataka watendaji
hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo na
kuzingatia maadili mema ya kazi.
0 comments:
Post a Comment