Pages

Ads 468x60px

Friday, July 8, 2016

Kitengo cha Dharura TANESCOchatakiwa kuongeza ubunifu



Mtaalam kutoka Kampuni ya Kuendeleza Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Nyaso Makwaya (kulia) akielezea shughuli za kampuni hiyo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini Prof. James Mdoe (wa pili kutoka kushoto) mara alipotembelea banda la TGDC.
Mtaalam kutoka Idara ya Madini, Wizara ya Nishati na Madini Philip Mathayo (kushoto) akitoa maelezo juu ya sera ya madini kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini Prof. James Mdoe (wa pili kutoka kulia) mara baada ya kuwasili kwenye banda la Wizara kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) Zena Kongoi (kulia) akielezea mikakati ya shirika hilo katika kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini Prof. James Mdoe (kushoto)
Meneja Uendelezaji Masoko na Teknolojia kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage (kulia) akimwonesha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini Prof. James Mdoe (katikati) matumizi ya majiko sanifu katika kupikia mara alipotembelea banda la REA. Kushoto kabisa ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Asteria Muhozya.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Ally Mluge (kulia) akielezea muundo wa shirika hilo kwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini Prof. James Mdoe (kushoto) mara alipotembelea banda la TPDC.


Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe amekitaka Kitengo cha Dharura cha Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kufanya kazi kwa ubunifu ili kukabiliana na malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi mara kwa mara.

Profesa Mdoe aliyasema hayo mara baada ya kufanya ziara katika banda la Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake katika Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa malalamiko ya wananchi juu ya ucheleweshaji wa huduma unaofanywa na kituo cha dharura cha TANESCO yamepelekea wananchi kuwa na taswira hasi juu ya shirika hilo. “Ninawataka kuwa wabunifu katika utendaji kazi wenu, kwa kutoa huduma kwa haraka kwa kuwa nyinyi ndio mliobeba taswira ya shirika,”alisema Profesa Mdoe.

Wakati huo huo akizungumzia sekta ya madini nchini, Profesa Mdoe alisema kuwa Serikali imejipanga katika kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwa wana mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP), Serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wa madini wanaokidhi vigezo. Alitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na kuwa na leseni za uchimbaji madini, kuonesha kuwa wanaendesha shughuli za uchimbaji madini pamoja na ulipaji wa kodi serikalini.

Alisisitiza kuwa Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ipo tayari kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia vifaa na mafunzo ili kukuza uzalishaji wa madini nchini na hivyo sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi .

0 comments:

Post a Comment

 
Blogger Templates