Taasisi
ya Serious Fraud Office ya Uingereza ( SFO ) inafanya mazungumzo na
Benki ya Standard Group ya Afrika ya Kusini Lakini iliyoorodheshwa
katika soko la hisa ya Uingereza ( London Stock Exchange ) ili
kumalizana kuhusu tuhuma za rushwa katika ununuzi wa hati fungani za
Serikali ya Tanzania yenye thamani ya dola za kimarekani milioni Mia
Sita ( $ 600m ). Mazungumzo hayo yanafanywa mbele ya Jaji katika mji wa
London.
Ndugu wanahabari, ni
jambo la kawaida kwa serikali yoyote duniani kuuza hati fungani. Mnamo
mwaka 2011/2012 Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliuza hati fungani (
Bonds ) zenye thamani ya dola za kimarekani 600 milioni ($600 million),
dhamana hizo za serikali zilinunuliwa na benki ya kigeni (Stanbic)
ambayo ni mali ya Standard Group ya Afrika ya Kusini, yenye makao makuu
yake huko London, Uingereza.
Hata
hivyo, sehemu ya fedha hizo haikuingia kwenye akaunti za Serikali ya
Tanzania na pia gharama za Bond hiyo zilipaishwa kupitia wakala wa kati
kati ( middle men ) na hivyo kupelekea rushwa ya takribani $60 milioni
kutolewa Kwa maafisa waliothibitisha biashara hiyo.
Ndugu
wanahabari, taasisi za kiuchuanguzi za nchini Uingereza, hasa ile ya
kushughulikia makosa ya rushwa (Serious Fraud Office-SFO) tayari
imeshafanya uchunguzi wake wa awali kwa kuhusisha pande zote
zinazohusika, na wamegundua kuwepo kwa rushwa kubwa katika mchakato huo,
jambo ambalo liliwafanya washauri uongozi wa benki hiyo hapa nchini
kuondolewa na kurejeshwa nchini Uingereza kwa hatua zaidi. Hata hivyo
SFO na Standard Group wanataka kulimaliza jambo hili Kwa mtindo wa
walivyomaliza suala la radar.
Ndugu
wanahabari, Chama changu cha ACT-Wazalendo, kinazitaka mamlaka za
kiuchunguzi hapa nchini, kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na upotevu wa
$600 milioni, ambazo kwa pesa ya Tanzania ni zaidi ya shilingi 1.2
trilioni. Hicho ni kiwango kikubwa sana cha fedha, ikilinganishwa na
makusanyo ya Mamlaka ya Maapato Tanzania (TRA). Tunaitaka Benki Kuu ya
Tanzania, FIU Tanzania na PCCB kuweka hadharani taarifa ya chunguzi zao
na kueleza ni kwanini hawajachukua hatua mpaka sasa.
Ndugu
wanahabari, chama cha ACT-Wazalendo, kinaunga mkono jitihada za Rais
wetu Dr John Pombe Joseph Magufuli, za kutumbua majipu, hivyo tungependa
kuona Mheshimiwa Rais akichukua hatua kwenye jambo hili ambalo lina
maslahi mapana ya nchi yetu, hasa ikizingatiwa na uzoefu tulionao katika
masakata kama hayo yanayohusisha nchi za kigeni, mfano mmojawapo ni
sakata la rada, ambalo vyombo vyetu vya uchunguzi vilisema hakukuwa na
rushwa, na baadaye serikali ya Uingereza ilithibitisha pasina shaka
kwamba kulikuwa na rushwa, na baadaye serikali yetu ilirudishiwa sehemu
ya fedha zilizozidi kwenye manunuzi ya rada ( chenji ya rada ).
Chama
cha ACT Wazalendo kinasubiri taarifa ya makubaliano ( settlement ) Kati
ya SFO na Benki ya Standard Group ( Benki mama ya Stanbic ) ili
kushauri zaidi hatua za kuchukua. Ikumbukwe kuwa Benki ya Stanbic ndio
ilihusika na kashfa ya Tegeta Escrow na mpaka sasa haijachukuliwa hatua
zozote kama ilivyoagizwa na Bunge. Benki hiyo imewaficha waliochota
fedha za escrow mpaka Leo.
( imesainiwa )
Masasi, 30 Novemba 2015
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
ACT-WAZALENDO
0 comments:
Post a Comment