* Atengua uteuzi wa Mwenyekiti
wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu TPA
* Amsimamisha kazi Katibu
Mkuu Uchukuzi
* Waziri Mkuu
awasimamisha kazi watumishi wengine 13 wa bandari
RAIS
Dkt. John Pombe Magufuli amevunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kutengua
uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari, Prof. Joseph Msambichaka pamoja na Mkurugenzi
Mkuu wa Bandari, Bw. Awadhi Massawe.
Dkt. Magufuli
pia ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaban Mwinjaka
kuanzia leo (Jumatatu, Desemba 7, 2015), na kwamba atapangiwa kazi nyingine.
Akitangaza
uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika leo ofisini
kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hatua
hizo zimechukuliwa kufuatia ziara mbili za kushtukiza alizozifanya katika mamlaka
ya bandari Novemba 27 na Desemba 3, mwaka huu.
Waziri Mkuu
amesema Rais Magufuli amevunja bodi hiyo na kutengua uteuzi wa viongozi hao kutokana
na utendaji mbovu wa muda mrefu wa Mamlaka ya Bandari na kwa kitendo cha viongozi
hao kutochukua hatua kwenye vyanzo.
Pia alisema
Katibu Mkuu amesimamishwa kazi kwa sababu ya kutosimamia kwa makini mashirika
mawili ya Bandari na Reli ambayo yako chini ya wizara yake ambako yeye mwenyewe
alizuru Shirika la Reli (TRL) Desemba 3, 2015 na kukuta kuna ubadhirifu wa sh.
bilioni 16.5/-.
“Tarehe 3 Desemba
mwaka huu nilifanya ziara ya kushtukiza pale TRL nikakuta wametumia visivyo sh.
bilioni 13.5/- walizopewa na Serikali. Pia nilikuta wamekopa sh. bilioni 3/-
kutoka benki ya TIB lakini nazo wamezitumia nje ya utaratibu. Fedha hizi
zilikuwa ni za kusaidia kuboresha miradi ya shirika lakini wao wamezitumia
visivyo. Uchunguzi bado unaendelea,” alisema Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha
kazi kuanzia leo viongozi watano wa sekta zilizotoa ruhusa ya makontena kutoka
ndani ya bandari pamoja na watumishi wanane wa bandari kavu ambao walihusika na
ukwepaji kwa makontena 2,387.
“Viongozi
hawa hawakuwemo kwenye ripoti ya ukaguzi lakini ni wahusika wakuu. Hawa ndiyo
waliotoa ruhusa ili makontena yaende kwenye ICDs. Nao ni aliyekuwa Meneja
Mapato ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu kitengo cha Fedha, Bw. Shaban Mngazija; aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha
na Mkuu wa Bandari Kavu (ICD) – ambaye amehamishiwa Makao Makuu kwa Naibu
Mkurugenzi Co-operate Services, Bw. Rajab Mdoe; Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Bw. Ibin
Masoud; na Meneja Bandari Msaidizi – Fedha, Bi. Apolonia Mosha
Pia
amewasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICDs) ambao ni Happygod
Naftari, Juma Zaar, Steven Naftari Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango
Alli, John Elisante na James Kimwomwa ambaye alihamishiwa Mwanza lakini kuanzia
sasa anasimamishwa kazi huko huko aliko.
“Bila wao
kuidhinisha hakuna kontena linaweza kutoka au kwenda kokote. Watumishi wote hao
wawe chini ya ulinzi na waisaidie polisi kupata taarifa hayo makontena ni ya
nani na yana thamani gani,” Waziri Mkuu alisema.
Waziri Mkuu
Majaliwa aliwaeleza waandishi wa habari kwamba Desemba 3, mwaka huu aliamua kurudi
tena bandarini kufuatilia na kuangalia hatua ya udhibiti wa upitishaji wa
bidhaa mbalimbali kinyume cha utaratibu. “Ziara yangu ilinipitisha hatua zote
za upitishaji mizigo ambazo pia kwa mujibu wa Taarifa ya Ukaguzi wa Ndani ya
tarehe 30 Julai 2015, Mamlaka ya Bandari iligundulika kuwepo kwa mianya mingi
ya ukwepaji kodi ikiwemo makotena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi – Septemba
2014 kinyume cha utaratibu”.
“Vitendo
hivi vinaonyesha kuwa bandari yetu hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa
kodi na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Serikali haitavumilia kuona watu
wachache au kikundi chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiibia Serikali
kwa namna yoyote ile kwa manufaa ya wachache kwani bandari ni eneo muhimu ambalo
likisimamiwa vizuri, linaweza kukusanya fedha nyingi na kuchangia Pato la Taifa,”
alisema.
Desemba
3, mwaka huu, Waziri Mkuu alimpa saa tatu tu Kaimu Meneja wa Bandari, Bw. Hebel
Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi
huo. Pia alimpa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha
mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye billing
system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment). Mwisho
wa kukamilisha zoezi hilo ni Desemba 11, 2015.
0 comments:
Post a Comment